Nasaka Mava ya Babu

Dunia iliwameza, majabari wa jamani,
Dunia ikatuliza, ikatwacha mashakani,
Dunia ikapuliza, makaburi upeponi,
Nasaka mava ya babu, fufue mizuka yake.

Walifunza ya Maisha, ya shubiri na ya uki,
Ya mwiko wakatupasha, yenye faraja na dhiki,
Viapo wakatulisha, na Leo hatusadiki,
Nasaka mava ya babu, fufue mizuka yake.

Walitafuna mihogo, na matunda ya kichaka,
Waliwafuga mifugo, kama ngamia na paka,
Hawakuzizua zogo, kwa kula nyama ya paka,
Nasaka mava ya babu, fufue mizuka yake.

Zamani zile za kale, kulikuwa na misimu,
Masika mvua tele, na jua lenye ugumu,
Hawakupiga kelele, kwa mavazi ya wazimu,
Nasaka mava ya babu, nifufue mizuka yake.

Sisahau ndoa yao, ndoa yao ya mitara,
Kumbuka watoto wao, wenye sawa sura zao,
Hawakutiana mbio, kwa ghasia za kukera,
Nasaka mava ya babu, fufue mizuka yake.

Waliishi kimlango, jamii ya waja wengi,
Walikuwa na mipango, kwa faida wao wengi,
Hawakupinda migongo, kupenda uvivu mwingi,
Nasaka mava ya babu, fufue mizuka Yake.

Walimwamini Jibana, Karima ndiye Mwuumba,
Walipenda kupendana, wakajua Mola Simba,
Ukweli hawakwezana, abudu hawakuumba,
Nasaka mava ya Babu, fufue mizuka yake.

© Mwangi wa Githinji
(malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!