Niepushie Beluwa

Mwaka umekamilika, shukrani kwake muumba
Naanza mwingine mwaka, goti chini nikiomba
Jazwe raha na fanaka, na siha nzuri sambamba
Ewe wangu Maulana, niepushie beluwa!

Ewe baba wa mbinguni, muumbaji wa milele
Mwakani Nipe amani, niepushie kelele
Amani ijae moyoni, nikuweke kwanza mbele
Ewe wangu Maulana, niepushie beluwa!

Kudusi unipe nguvu, kazini nikaze buti
Uniepushe maovu, kazini nipate noti
Unipe uvumilivu, nifanye kazi kwa dhati
Ewe wangu Maulana, niepushie beluwa!

Safari hii ni ndefu, naomba uwe na mimi
Uniepushie rafu, ndani yako nijihami
N’takuita mara alfu, moyoni na kwa ulimi
Ewe wangu Maulana, niepushie beluwa!

Moyo wa kusamehea, unipe wangu kudusi
Pate kuwasamehea, walojawa matusi
Amani naiombea, nisije nikakuasi
Ewe wangu Maulana, niepushie beluwa!

© Justine Bin Orenge

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!