Ndevu za Kijivu

Busara kitu adimu, adimu kwao vijana,
Haya maneno si ndimu, ndugu elewa maana,
Maneno mengi ni sumu, usipende kugombana,
Mwenye ndevu za kijivu, kimwona mpe staha.

Akifumba yalo fumbo, ng’anga’na na ufumbue,
Akipiga ya mgambo, ombi langu ukimbie,
Ulijue hilo jambo, maanani utilie,
Mwenye ndevu za kijivu, kimwona mpe staha.

Akitega tendawili, tegulia kwa makini,
Akisemea methali, ikulee maishani,
Ukionywa kwa ukweli, usipende uongoni,
Mwenye ndevu za kijivu, kimwona mpe staha.

Akushikishe sikio, nawe vyema ulitege,
Akikupa ufunuo, nawe usikuwe bwege,
Usimpe mkupuo, kumrusha kama ndege,
Mwenye ndevu za kijivu, kimwona mpe staha.

Akisemea methali, itafutie maana,
Na kwa zako zote hali, maisha ni kusomana,
Upige hatua mbali, ‘sijali’ wanosemana,
Mwenye ndevu za kijivu, kimwona mpe staha.

Agane zake hadithi, ngano zisizo na mwisho,
Busara nayo urithi, pate nyingi hamasisho,
Hekima nayo kurithi, milele Leo na kesho,
Mwenye ndevu za kijivu, kimwona mpe staha.

© Mwangi Wa Githinji
(malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!