Kijacho Kinapokuja

Mui bado kuwa mwema, hutenda likatendeka,
Hanalo la taadhima, kwa hilo akapendeka,
Ni kwa ovu amevuma, tena kuwa msifika,
Kijacho kinapokuja, ni kijasho humjia!

Ameshauriwa sana, mgumu kuambilika,
La sitara ndilo hana, kwa hilo kafahamika,
Hili zimwi likiguna, waoga hutetemeka,
Kijacho kinapokuja, ni kijasho humjia!

Akumbukwapo asemwe, husemwa akasemeka,
Hanaye mwandani kamwe, usidhani apendeka,
Umati humwoni pamwe, wote wamebusurika
Kijacho kinapokuja, ni kijasho humjia!

Atasema akuseme, akusimange kufoka,
Tena mara akulime, pamoja na kukufyeka,
Hawi kwa wema avume, ila wingi wa dhihaka,
Kijacho kinapokuja, ni kijasho humjia!

Jamii imemjuwa, kabaki kusononeka,
Woga ni kumtunguwa, tena akakosoleka,
Hubaki kumchambuwa, wakibaki kusumbuka,
Kijacho kinapokuja, ni kijasho humjia!

Kwa jema hana ridhaa, hiari hulazimika,
Mja hutifua baa, mandhari kuchafuka,
Tena hufanya hadaa, vituko kila dakika,
Kijacho kinapokuja, ni kijasho humjia!

Halumbi pawapo heri, hapendi kuneemeka,
Huyu ni mja wa shari, apendaye mieleka,
Ni adui wa mazuri, mui asebadilika,
Kijacho kinapokuja, ni kijasho humjia!

Haridhishwi na muwanga, pawapo kiza hutoka,
Tena hawapo kupanga, lijalo likatendeka,
Walio wema hulenga, ni mja kindengereka,
Kijacho kinapokuja, ni kijasho humjia!

© Kĩmani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!