Nakuonya Mlima Kenya

Mzalendo anaonya, kusimanga yako dhima,
Kwa hali umejifanya, ukaringia kuvuma,
Wengine kakukanganya, Kilimanjaro ki wima,
Naonya Mlima Kenya, kudharau vijilima!

Kupenya ulikopenya, wengine wamejitoma,
Mengi umeyamenya, twabaki kushika tama,
Shadidi umejifanya, hatunalo la kusema,
Naonya Mlima Kenya, kudharau vijilima!

Inuka ukafunganya, ujue vilivyovuma,
Mwengine kakudanganya, ola mvumo wa ngoma,
Usidhani kutapanya, hukufanya kuwa mwema,
Naonya Mlima Kenya, kudharau vijilima!

Mlima Suswa u Kenya, twautambua mlima,
Unazidi kuusinya, usijue warindima,
Wasema ni kubambanya, ufundi wawaandama,
Naonya Mlima Kenya, kudharau vijilima!

Swifa umewapokonya, kwa lengo la kuwazima,
Hawashindi ndovu kunya, misamba itawakwama,
Kwengine wajikusanya, waushinde kusimama,
Naonya Mlima Kenya, kudharau vijilima!

Usimtazame panya, udhani hana mtima,
Tena chake kupokonya, takuwa huna huruma,
Mlima ninakukanya, uliwate la hujuma,
Naonya Mlima Kenya, kudharau vijilima!

© Kĩmani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!