Tukemee Sadarusi

Naja pasi nayo hodi, Njiwa wenu muwadhama,
Nidadavuwe hadidi, pasi kukwama kutwama,
Kunena imenibidi, mazingira’we salama,
Karatasi sadarusi, tukemee kwayo fujo.

Madhara mengi jamani, kutaja nitagusia,
Mosi magonjwa tumboni, wanyama kitafunia,
Mwisho wandani kifoni, hasara tunabakia,
Karatasi sadarusi, tukemee kwayo fujo.

Pia urembo hatuna, zikiwa kila mahali,
Uchafu ni kubanana, kawa bovu ja ajali,
hewa swafi hatunana, uzima kuukabili,
Karatasi sadarusi, tukemee kwayo fujo.

Sura mbaya taifani, kwa sana zikioneka,
Zikiwa kote mitini, suretu kuharibika,
Tuzamie aibuni, tuue jina hakika,
Karatasi sadarusi, tukemee kwayo fujo.

Hewa piya zachafua, zikichomwa mabiwini,
Maradhi tunaugua, mili nje piya ndani,
Habuta tunaing’oa, hatima yake mavani,
Karatasi sadarusi, tukemee kwayo fujo.

Kalamu naweka Chini, rangi imeniishia,
Tuzimalize jamani, taifa safi salia,
Ujumbe nimewapeni, lenu ni kuzingatia,
Karatasi sadarusi, tukemee kwayo fujo.

© Sauti Ya Njiwa
Little Friends Academy, Naivasha

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!