Nchi Yetu

Nchi yetu kaumbika, ka nini yafananika,
Kila pembe kimlika, yametameta hakika,
Ni wazi inasifika, Ulaya na Amerika,
Si sote tuunganeni, Kenya yetu isongeni.

Riadhani twasifika, mataji tumeyasaka,
Ya Uchina name Osaka, tumeshinda bila shaka,
Kemboi na Rundishika, mlitamba kwa hakika,
Si sote tuunganeni, Kenya yetu isongeni.

Kandanda kiangazika, Wanyama anasifika,
Manchesita wateseka, Viki awatingizika,
Olunga moto awaka, Hispania bila shaka,
Si sote tuunganeni Kenya yetu isongeni.

Utalii kiumulika, Ulaya twatambulika,
Masai Mara kifika, utafurahi hakika,
Bahari Hindi kifika, tabarizi bila shaka,
Si sote tuunganeni, Kenya yetu isongeni.

Kilimo kiangazika, kileleni tumefika,
Chai yetu ni hakika, duniani twatajika,
Katari na Jamaika, ubabe wetu mefika,
Si sote tuunganeni, Kenya yetu isongeni.

Rais wetu Ibuka, Mola akupe baraka,
Kenya yetu yasifika, juhudi zako hakika,
Twasongambele hakika, dunia twatambulika,
Si sote tuunganeni, Kenya yetu isongeni.

Kadi tamati hewaka, kwa sasa naondoka,
Nataraji kayashika, niloweleza hakika,
Nchi yetu tasifika, yalomema tayadaka,
Si sote tuunganeni, Kenya yetu isongeni.

© Kamwara Eric Kimathi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!