Mke Wangu

La kwanza ni Muriungi, mwana wa kwanza wa Mwiti,
Nalo jina la utungi, kinywa cha mamba sing’ati,
Sio mja wa shangingi, wala kizungumkuti.

Wa kwanza nilimuowa, mke mufti mufti,
Kwa huba nilizidiwa, hoi kaapa simwati,
Mpole kushinda njiwa, kasema nina bahati.

Ndipo alinishitua, jikoni ni zuzu eti!
Jama akikupikia, we kumsuta husiti,
Chakulache cha udhia, kukila raha hupati.

Huyo nikamtaliki, wa pili kwangu kaketi,
Uzuriwe husemeki, upishi so atiati,
Halima kipika keki, tala upasuke eti!

Naye kangiya dosari, hanipi la mahututi,
Penzi lake sio zuri, japo yeye baithati,
Akaanza leta shari, mambo ya uasherati.

Nikaja naye Amina, mwenye mapenzi ya dhati,
Vyakulavye kiviona, utamu wa chokoleti,
Amina alifanana, na wa peponi banati.

Ndipo ikabisha shaka, akajifanya gazeti,
Mmbea katambulika, muwenezaji ghalati,
Lipofika yalofika, nusura niwe hayati.

Nikatukua Aisha, wa kijiji cha Songeti,
Wa aya zisizoisha, kwa jirani humpati,
Penzile halikuchosha, hata kwa ukarabati.

Kumbe jijini mgeni, mshamba chafu hafuti,
Hapasafishi nyumbani, uvundo raha huvuti,
Kanaibisha jamani, na kunipa kibuhuti.

Ndipo kajiamuliya, niwarejeshe sharti,
Shike pake kulla ‘moya, kulea nijizatiti,
Sasa twaishi pamoya, taabu hainipati.

© Muriungi Martin
Sauti kuu. Kinywa cha mamba.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!