Tuishipo Duniani

Tuishipo duniani, natuishi kufaana,
Tuishipo duniani, ‘sikubali paruzana,
Tuishipo duniani, natuishi kubebana,
Sisi sote tuko sawa.

Tuishipo duniani, tuishini kwa amani,
Tuishipo duniani, chuki tuikataeni,
Tuishipo duniani, tupendaneni jamani,
Sisi sote tuko sawa.

Tuishipo duniani, ‘saidiana kubali,
Tuishipo duniani, nijali namikujali,
Tuishipo duniani, tupane njema kauli,
Sisi sote tuko sawa.

Tuishipo duniani, tutimize zetu ndoto,
Tuishipo duniani, tusipigane kwa fito,
Tuishipo duniani, tuelewe ni mapito,
Sisi sote tuko sawa.

Tuishipo duniani, tuwache ugumegume,
Tuishipo duniani, fitina nyingi tukome,
Tuishipo duniani, kinyongo chetu tuteme,
Sisi sote tuko sawa.

Tuishipo duniani, kaburi tutaingia,
Tuishipo duniani, kimya ndani tabakia,
Tuishipo duniani, mifupa itasalia,
Sisi sote tuko sawa.

Tuishipo duniani, utengano tukemee,
Tuishipo duniani, wamoja natusalie,
Tuishipo duniani, umoja tukubatie,
Sisi sote tuko sawa.

© Joseph Mwangi
Sauti ya Njiwa
Naivasha

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!