Buriani Njoroge

Mashariki lachomoza, kuuleta wake mwanga
Nayo nuru yatandaza, tumaini la mganga
Ghafla laingia giza, ipi sisi yetu nanga
Lako lengo litimiza, ulale pema Njoroge.

Metuacha kwa majonzi, twalia si wanagenzi
Ndugu zako na wazazi, wamejawa na simanzi
Hukuimaliza kozi, umeenda kwa Mwenyezi
Mwenyezi akurehemu, shujaa wetu Njoroge.

Wamekuua kinyama, kwa mtutu wa bunduki
Upo wapi usalama, ama ni semi lukuki
Laana takuandama, muuaji kwa bunduki
Litenda wema Njoroge, Mungu mlaze peponi.

Likuwa kifua mbele, kututafutia haki
Uongozi wa upole, Rabana akubariki
Tutazipiga kelele, hadi tuipate haki
Kidero ulale pema, Mola tujaze subira.

Ipo wapi serikali, nawe waziri Amina
Chukua hatua kali, kwa uongozi wa lana
Uonekane ukweli, wa zetu hizi lalama
Wangila utuongoze, mambo yetu yawe bomba.

Naja kwako Boineti, tueleze haya vyema
Umekikalia kiti, na hakuna usalama
Mevalia hilo koti, polisi kawa mnyama
Tunataka yetu haki, kwa nguli wetu Njoroge.

Tumwekeni maombini, mwendazake mwanagenzi
Tupe faraja Manani, wakati huu wa dhiki
Kalamu naweka chini, kwani lanitoka chozi
Twakutamani Kidero, lala pema Njoroge.

Mengi mimi nimesema, nisije nikakufuru
Matendo yako ni mema, Rabana twakushukuru
Ulimwita kwako kwema, wako wote utukufu
Mlaze pema Njoroge, ndilo ombi letu Mola.

Tunaringa tuna nini, sote tukifa twanuka
Sote pia tu njiani, tutaenda kwake Mola
Tayari jama tuweni, kwa kumsifu na sala
Litimiza lako lengo, ulale pema Njoroge.

©Emmanuel Charo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!