Kimahaba Sioni

Nikuambie halua, zuri lililo moyoni
Nakupenda wangu ua, sitokwacha asilani
Mimi nimekuchagua, uzuri uso kifani
Kimahaba sioni, ni kipofu mapenzini

Sura yako ya utoto, nikwamba unaniita
Ulimi ulomikunjo, kwa manenoye yanata
Kifua chenye vidodo, hakika wanikamata
Kimahaba sioni, ni kipofu mapenzini

Kiuno chako cha nyigu, cha utamu hauishi
Membamba yako miguu, kikukosa sitoishi
Nakuomba unijibu, niwanyamaze wabishi
Kimahaba sioni, ni kipofu mapenzini

Ninahisi tena njaa, lakini si ya chakula
Nina kiu lonijaa, kwa maji haitoisha
Kwa mapenzi meduwaa, njoo unipe furaha
Kimahaba sioni, ni kipofu mapenzini

Urembo kakupa Mola, sifa anastahili
Uzuri wako kimwana, waweza vunja jabali
Napagawa kikuona, siwezi stahimili
Kimahaba sioni, ni kipofu mapenzini

Tamati nimeshafika, nishakupea wasia
Kimwana unasifika, ombi umelisikia
Hima hima nimechoka, jama nisije zimia
Kimahaba sioni, ni kipofu mapenzini

© Emmanuel Charo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!