Sote Wana wa Adamu

Kaka dada unadini, mimi pia muamini
Wenda msikitini, jumaa uibadani
Kanisani waumini,kumshukuru Manani
Dini zisitugawanye, sote wana wa Adamu

Mungu akatuletea, mitume watuongoze
Dini wameizoea, ili watuelekeze
Nasaha watatupea,jamani tusiwabeze
Dini zisitugawanye, sote wana wa Adamu

Tu viumbe wa Jalali,sababu tumefanana
Akatupea vibali, tuishi kwa kufaana
Tuyavunje majabali,, kwa moyo wa kupendana
Dini zisitugawanye, sote wana wa Adamu

Tunaringa tuna nini, sote tukifa tukifa twanuka
Tumwombe wetu Manani, atupe zake baraka
Tusibaki unyongeni, ila tusiwe vibaka
Dini zisitugawanye, sote wana wa Adamu

Kikomo nimefikia, wacha nikale boboro
Nikikosa sitolia, nitabugia kiporo
Kwa wasio nitambua, ni wenu malenga Charo
Dini zisitugawanye, sote wana wa Adamu

© Emmanuel Charo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!