Viumbe Wameibana

Ulimwengu mzunguko, na waja kama siafu,
Na malaika waliko, wangaliye watukufu,
Watulinde kama koko, Sisi viumbe hafifu,
Jamii iliyo pana, viumbe wameibana.

Kaskazi mashariki, duniani pande zote,
Rasilimali ya haki, iliyopo potepote,
Wachache wenye mikuki, wachukuye mali yote,
Jamii iliyo pana, viumbe wameibana.

Jamii pasi wachache, yalilia ufukara,
Wachache mali wafiche, kwa kuwa wameyapora,
Jamii na waiache, hasira pasi hasara,
Jamii iliyo pana, Viumbe wameibana.

Na matumbo yasoshiba, wachache kwenye jamii,
Wafanyalo ni kuiba, kunyanyaza wa bidii,
Na milele kuwaziba, wanyonge hawasikii,
Jamii iliyo pana, viumbe wameibana.

‘Kiwa nayo mamlaka, kuzungukwa na kiburi,
Kujiona kwa hakika, kama kweli wenye heri,
Walowapa mamlaka, kujuta bila hiari,
Jamii iliyo pana, viumbe wameibana.

Bila shaka utengano, kati yao uliopo,
Hawana uhusiano, kama wanyama na popo,
Wanyonge kuzibwa neno, kubaki pale walipo,
Jamii iliyo pana,Viumbe wameibana.

Jamii basi kuoza, utengano kikithiri,
Walosoma kutoweza, ‘pata kazi kwa hiari,
Wengine hata kuuza, milio pasi hiari,
Jamii iliyo pana, viumbe wameibana.

Naelekea tamati, kikomo nitakiweka,
Ntazieka hizi hati, uovu tutauzika,
Tukaweke harakati, jamii kutoizika,
Jamii iliyo pana,Viumbe wameibana.

Uovu tuondoeni, jamii ikuwe sawa,
Umoja tuuimbeni, ‘tengano umee bawa,
Umoja tuuimbeni, milele tukuwe sawa,
Jamii iliyo pana, viumbe wameibana.

Haya basi nawaaga, asante na kwaherini,
Viongozi twawaiga, timbwikwiri wachaneni,
Jamii ninawaaga, na Mola awalindeni,
Jamii iliyo pana, viumbe tusiibane.

© Robinson Obaigwa

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!