Asali Kuwa Shubiri

Nalo jambo lanikera, hivi leo nalinena,
Dunia imeparara, kwa maovu ya vijana,
Wazee wenye vipara, wanawachelea wana,
Asali jama ni chungu, utamu kawa shubiri.

Ngono kawa biashara, kinyume na zetu dini,
Hasa pwani hadi bara, wauliza bei gani,
Wamejaa mahawara, kila kona vilabuni,
Asali jama ni chungu, utamu kawa shubiri.

Hakuna tena cha ndoa, hivi sasa hofu tele,
Zilizopo zina doa, ka uchafu kwa mchele,
Magonjwa yatuondoa, ukimwi hadi upele,
Asali jama ni chungu, utamu kawa shubiri.

Misikiti makanisa, msaada upo wapi?
Elimu iliyo sasa, faidaze ziko wapi?
Kila uchao mikasa, itikadi ziko wapi?
Asali jama ni chungu, utamu kawa shubiri.

Tuwapeni nasaha, vijana wabadilike,
Dini zitoe usia, kwema waelekee,
Wana waache madaha, ili wasiwe wapweke,
Asali jama ni chungu, utamu kawa shubiri.

Ukingoni nimefikia, bado nasisitizaa,
Chovya chovya kikushika, shubiri pia utachovya,
Ukimwi umesifika, hakika umesambaa,
Asali jama ni chungu, utamu kawa shubiri.

© Emmanuel Charo (Malenga Daktari)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!