Menimwaga Kama Mchele

Nimetambua ukweli, wa usemi wa zamani,
Umdhaniaye kweli, hakika siye jamani,
Kumkosa huyu mwali, ambaye namtamani,
Menimwaga ka mchele, ndo kuku wanidondoe.

Nilidhani nimepata, kumbe nimepatikana,
Kisura wameremeta, kwa nini umenikana,
Nimekuwa ka zezeta, lini tutarudiana,
Menimwaga ka mchele, ndo kuku wanidondoe.

Tiara mi nimekuwa, napepea kwa mawazo,
Takataka nimetupwa, kwa wangu wingi uozo,
Mapenzi kama utumwa, ama ya kifaurongo,
Menimwaga ka mchele, ndo kuku wanidondoe

Usoni nina huzuni, mtimani tabu tele,
Damu yavuja moyoni, donda ndugu si upele,
Meniacha mashakani, ka Brazili kwa pele,
Menimwaga ka mchele, ndo kuku wanidondoe.

Macho yako ya kikombe, cha nyigu chako kiuno,
Mwendo wako wa kobe, ya upanga yako shingo,
Acha nibugie pombe, nikutoe kwa ubongo,
Menimwaga ka mchele, ndo kuku wanidondoe.

Tabibu umeniacha, kwa hali ya mahututi,
Usinipe yako picha, nakuona ka baruti,
Acha nipike mchicha, ninywe chai kaimati,
Menimwaga ka mchele, ndo kuku wanidondoe.

© Emmanuel Charo (Malenga Daktari)
Meru University