Haki Yangu Kuchagua

Sumilani majagina, msaada nawaomba,
Nasaha zatakikana, kwangu kijana wa shamba,
Fesibuku liniona, akataka zangu namba,
Nisikizeni wazazi, penzi hili lanimaliza.

Sikuiona sababu, namba zangu kumnyima,
Nikidhani tanitibu, kiu kichonisakama,
Nikafanya taratibu, ili nimwahi mapema,
Nisikizeni wazazi, penzi hili lanimaliza.

Wazee walikataa, pindi tu walipomwona,
Banati alivyovaa, karibu kutoa lana,
Wakasema hatozaa, nikioa wanikana,
Nisikizeni wazazi, penzi hili lanimaliza.

Nilipo ni njia panda, msiniache naomba,
Ama nijivishe sanda, Mara nigeuke kimba,
Ona mawingu yametanda,siyawezi ninaamba,
Nisikizeni wazazi, penzi hili lanimaliza.

© Moses Chesire (Sumu ya Waridi)