Mihadarati Sithubutu

Njiwa naja kuwaonya, msikizi nisikize,
Baba, mama pia nyanya, babu bali sinicheze,
Afya zenu kutosinya, shika ndewe niweleze,
Mihadarati kaburi, kutumia sithubutu.

Mbangi, pombe na miraa, situmie asilani,
Kitumia tazubaa, uchaa wa ubongoni,
Yenu yote talemaa, hatimaye mtangani,
Mihadarati kaburi, kutumia sithubutu.

Vita tazidi nyumbani,madawa kiyabugia,
Muishie zahamani,hasara kujizolea,
Kesha muwe laitini,wendani kiwapotea,
Mihadarati kaburi,sithubutu kutumia.

Nisemayo kipuuza,nisikize kwa hakika ,
Kazi yako tapoteza,ubaki kuhangaika,
Mwenyewe utajiliza,matozi yasofutika,
Mihadarati kaburi,sithubutu kutumia.

Isitoshe nayo hadhi,kwa fujo tajishushia,
Waja kuone mpudhi,kuheshimu asojua,
Soni utajikabidhi,ushindwe kuibukia,
Mihadarati kaburi,sithubutu kutumia.

Sithubutu kutumia, beti zangu nikibana,
Kwa sauti narudia, dawa hizi huuana,
Usalama kimbilia, kwaye Rabi Subahana,
Mihadarati kaburi, sithubutu kutumia.

Mwalimu Mwangi,
Sauti ya njiwa,
Naivasha.