Kugoma Sioni Tiba

Naanzia na Jalia, jina lake kulisifu,
Nishati kunijalia, nabarakaze sufufu,
Manesi kiwandikia, nipe mizani Raufu,
Kugoma tiba sioni, nasonona na kulia.

Nasonona nakulia, kitazama vitandani,
Nabaki kujimakia, wauguzi mnanini,
Huruma kuiachia, mmekiri midomoni,
Kugoma tiba sioni, suluhu katu sioni.

Suluhu katu sioni, kuachia waja kufa,
Huno ni uhayawani, kidhania bora sifa,
Mwogopeni Rahimani, nesi uzibeni ufa,
Kugoma tiba sioni, ipunguzeni presha.

Ipunguzeni presha, tupunguzie makali,
Njaa ndo yasababisha, lipimeni kwa ratili,
Kugoma mseme tosha, kutulia kakubali,
Kugoma tiba sioni, wauguzi shika jembe.

Wauguzi shika jembe, karejeeni kazini,
Hata mkilipwa embe, litieni mfukoni,
Wapeni wagonjwa tembe, tawabariki Manani,
Kugoma tiba sioni, ivuteni nasubira.

Ivuteni na subira, ipo siku ya furaha,
Yawaishie madhira, ishuke nyota ya jaha,
Iwafikie kudura, maisha yawe tufaha,
Kugoma tiba sioni, naukemea mgomo.

Naukemea mgomo, unondelea ntini,
Wauguzi toka omo, mwahitajika ngamani,
Katu sio domodomo, naomba nielewani,
Kugoma tiba sioni, hapa mwisho nakomani.

© Mwalimu Mwangi (Sauti Ya Njiwa)
Naivasha