Zinduka Mkenya

Hebu acha kuzubaa, si Wakenya tunapaa,
Kokote tunang’aa, Sifa bora tumetwaa,
Pepo lipi limekuvaa, we hutaki kutufaa?
Kwetu vema tumekaa, na hatutaki balaa.

Warandaranda mitaa, kwa porojo na papara,
Kwa uwozo na hadaa, jina letu walichora,
Ukabila wazagaa, ni udhia na hasara
Kwetu vema tumekaa, na hatutaki balaa.

Yetu kura yanukia, viongozi kuchagua,
Kwa busara tachangia, au tungu tatumbua?
Matusi twayachukia, Kenya yetu familia,
Kwetu vema tumekaa, na hatutaki balaa.

Hebu mkenya tulia, tusemezane kwa nia,
Ili tusije kulia, jipange si kudhania,
Rungu mawe tupilia, kikupa eti tumia,
Kwetu vema tumekaa, na hatutaki balaa.

Ndugu hebu  uza sera, si kwa fujo kutukera,
Mihela yako fikira, haki uje kutupora,
Tukajawe na hasira, tujilize kila mara,
Kwetu vema tumekaa, na hatutaki balaa.

Tuacheni uhasama, Kenya yetu iwe wima,
Ikibidi ukachoma, heri ukachome nyama ,
Kama kupiga lazima, piga kura ya salama,
Kwetu vema tumekaa, na hatutaki balaa.

Wana tunayo tamaa, mbeleni kwetu kung’ara,
Viongozi kiandaa, wenye utu na busara,
Uso sije kuchakaa, tusalie matambara,
Kwetu vema tumekaa, na hatutaki balaa.

Ndugu zetu twawapenda, ngazi pamoja tapanda,
Sisi bado tu makinda, tafurahi kitulinda,
Mbele sote tunaenda, wenye kicho twawashinda
Kwetu vema tumekaa, na hatutaki balaa.

© Okelo Wesonga (Malenga Mtafunamiwa)