Namba Nawe Maulana

Namba nawe Maulana, goti nimekupigia,
Naja nikisinasina, machoni mekulilia,
Na’lilia nguvu sina, kwako nimenyenyekea,
Nakuwa kifefe ona! Nguvu zinaniishia,
Nakuomba Maulana, ndani yangu kuingia.

Namba nawe Maulana, chini nimeinamia,
Nami mekukosa sana, mbali nilikukimbia,
Nami nilikosa sana, mekumbushwa na dunia,
Nalo kamwe singefana, anasa linihadaa,
Naomba kurudiana, upendo kurejelea.

Namba nawe Maulana, dunia ya sumburua,
Nateseka Maulana, kuwa mbali najutia,
Na mabaya nimeona, kaichukia dunia,
Narudi mwanao tena, moyo wangu mefungua,
Narudi mwanao tena, nyumbani ninarejea.

Namba nawe Maulana, imenifunza dunia,
Nakuhitajiya Bwana, mateso kunondokea,
Nataraji uje Bwana, mwanao kunikomboa,
Natarajia kupona, penzilo likirejea,
Naja kwako Maulana, mtimani naungua.

Namba nawe Maulana, muovu kanivamia,
Najaribu nang’ang’ana, siwezi kujikomboa,
Na damu imegandana, kitete kimeningia,
Nakutaka ewe Bwana, mabawa kuniwingia,
Nakuhitajiya Bwana, joto lako kunipea.

© Justine Bin Orenge