Anyango Binti Okumu

Kuna mmoja banati, Anyango Binti Okumu,
Kusema naye bahati, hata iwe kwa salamu,
Leo natikiza njiti, niseme nitoe hamu,
Niparuze kiberiti, ‘wake moto au bomu.

Kuwa naye nilitaka, mipango kapombojea,
Nduli wangu kapendeka, moyoni nikaumia,
Upepo kababaika, damu nikamlilia,
Mzigo kanibandika, Nina kikomba cha njaa.

Lakini hakuelewa, kwake nilisalitika
Kwini nilimwona njiwa, kwangu moyoni kafika,
Nilipokunywa kahawa, kikombeni unicheka,
Kinda kamkumbatiwa, japo wakufikirika.

Anauteka mtima, huyu banati Anyango,
Napenda bila kusema, tavamia kwa mpango,
Kwa nje Nitausukuma, ila kantilia pingo,
Hata siweze sukuma, nitauvunja mlango.

Kama fisi nadoea, udenda ukinitoka,
Kwini namtamania, Binti alo kaumbika,
Kila siku namwazia, moyoni nimetekeka,
Kipata ‘tafurahia, moyo utatulika.

© Justine Bin Orenge