Kisura Kindengereka

Wapi nilipotazama, mtima nilipokupa?
Ningelijua mapema, kamwe nisingelikupa,
Umeuchezea mama, sasa roho inapapa,
Kisura Kindengereka, moyoni sikutamani

Dada wacha kukimbia, pande zote duniani,
Huna unalolijua, maishani Limbukeni,
Maisha wayavamia, utajifundisha lini?
Kisura Kindengereka, moyoni sikutamani

Nasema sikutaki, sikutaki nyambovu,
Yako hayafikiriki, unayotenda maovu,
Kimwana hutamaniki, mekosa uvumilivu,
Kisura Kindengereka, moyoni sikutamani.

Umekuwa kidubwasha, umekosa thamani,
Kiberiti umewasha, kitakachozima nini?
Usijitie mapresha, katulie maishani!
Kisura Kindengereka , moyoni sikutamani.

Kwako nimepapatuka, kamwe sitarudi tena,
Kwangu umekuwa taka, sitakutamani tena,
Gogoo sitaitaka, kwako nitamani tena,
Kisura Kindengereka, Moyoni sikutamani

© Justine Bin Orenge