Dawa ya Mvuto

Mi mganga nina dawa, ya kuongeza mvuto
Inakuweka u sawa, ung’ale ng’ale ka vito
Ufanye watu kuowa, nitie upepo puto
Nina dawa ya mvuto, tulia upawe dawa

Kutinda watinda nyusi, weka za mbuzi kope
Mvuto sio mahipsi, dukani wende ukope
Mikucha kama ya pusi, utanasa kwenye tope
Nina dawa ya mvuto, tulia upewe dawa

Mvuto si ulimbwende, watu husaka akili
Safari pamoja mwende, macho yaonayo mbali
Utamu wote wa tende, jangwani hustahimili
Nina dawa ya mvuto, tulia upewe dawa

Kauli nayo ni dawa, weka hili akilini
Busara ni kama chawa, wape makazi kichwani
Ulimbukeni kutuwa, utilie maanani
Nina dawa ya mvuto, tulia upewe dawa

Si dawa ya sumbawanga, au mganga wa tanga
Si mizizi ya kutwanga, hilo mie sijalenga
Tamaa ikikutinga, wageuka ja mjinga
Nina dawa ya mvuto, tulia upewe dawa

© Onesmo Joel