Jibwa Litaniumia Toto

 

Ninautoa uneni, nieleze kwa uketo,
Niitangaze ilani, limenijia fukuto,
Nitafute wa kughani, mlidake kwa fumbato,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Naeleza hadharani, sielezi kwa mkato,
Hili jambo halifani, natangaza wangu mwito,
Hakuna raha nyumbani, imezidi rangaito,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Natishwa na hayawani, apendwaye kama vito,
Nakosa la kuamini, hali hii ya mpwito,
Nimewaza kwa makini, usinipate mvuto,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Litajificha uani, kulia ama kushoto,
Lishambulie mgeni, na yeyote kwa mseto,
Ukilipata pembeni, hukosi kuona moto,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Hutalikosa langoni, linao upana mato,
Halinalo la utani, linaisaka mipito,
Heri niwe silioni, nayahofia majuto,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Sinayo mengi mapeni, akatibiwe mtoto,
Fimbo tawa mkononi, bakora ama ufito,
Nikiviwacha chumbani, jibwa taligonga ngoto,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

Mwanangu namthamini, ni kama langu liwato,
Nitamlinda yakini, asitumie magwato,
Asijipate shakani, limzidie kunyato,
Hili jibwa la jirani, litaniumia toto!

© Kimani wa Mbogo