Nyanya Njema

Mwafulani sikiliza, nikupashe ukajuwa,
Leo sitanong’oneza, kinywa changu tapanuwa,
Jambo hili kuliwaza, utaweza fafanuwa,
Nyanya njema yapendeza, sokoni hutamaniwa.

Wamevuna walokuza, wateja kuanikiwa,
Yang’aa hata kwa kiza, wateja wamegunduwa,
Wengi wamejitokeza, sokoni kuinunuwa,
Nyanya njema yapendeza, sokoni hutamaniwa.

Mekomaa imejaza, sokoni yatambuliwa,
Hijavunda ikaoza, rangi yake yapendewa,
Kwa wemae yajiuza, urembo yafurahiwa,
Nyanya njema yapendeza, sokoni hutamaniwa.

Rekodi imeziweza, imebaki kusifiwa,
Wima imejitokeza, ipate kununuliwa,
Hini hijajitembeza, juani hijaunguwa,
Nyanya njema yapendeza, sokoni hutamaniwa.

Watu mate wanameza, tamaa kuwasumbuwa,
Wapo ilowapumbaza, japo hitaki kuliwa,
Ukomavu metimiza, nyanya ikazubaiwa,
Nyanya njema yapendeza, sokoni hutamaniwa.

Wateja huitukuza, hata goti kupigiwa,
Kila mja huuliza, maswali asojibiwa,
Nyanya imejitangaza, maelezo ikatowa,
Nyanya njema yapendeza, sokoni hutamaniwa.

Vidudu vinaiwaza, japo hijaharibiwa,
Nyanya imeshaongoza, wema mwingi imejawa,
Uzuri hijapoteza, sifa imeshapatiwa,
Nyanya njema yapendeza, sokoni hutamaniwa.

© Kimani wa Mbogo