Lumba Utifue Vumbi

Hunyamazi kuwa simba, nayo lugha huipambi,
Hutungi unavyoyumba, wala kwa tungo hufumbi,
Waamua kuwa chemba, na kwa maneno huchimbi,
Huambi wala kuimba, lumba kutifua vumbi.

Kujifungia kwa chumba, ya kipaji huyakumbi,
Isiwe tu wajigamba, pasipo kuja ukumbi,
Mkulima ni kwa shamba, hendi kuokota simbi,
Huambi wala kuimba, lumba kutifua vumbi.

Si kwa umbo uwe mamba, lakini nyama hulambi,
Usibakie kutamba, na hufui hata numbi,
Kipaji umekitimba, hicho chako hukirembi,
Huambi wala kuimba, lumba kutifua vumbi.

Unazidi kujigamba, ukabaki u sombombi,
Unavyolia kuwamba, ni kheri utubu dhambi,
Alichokupa Muumba, haifai kukifumba,
Huambi wala kuimba, lumba kutifua vumbi.

Shida zinavyokusomba, kwako zimepiga kambi,
Mengi yanavyokukumba, unakumbuka maombi,
Unajipuuza mwamba, hujui unalo tumbi,
Huambi wala kuimba, lumba kutifua vumbi.

© Kimani wa Mbogo