Yabidi Nitarazaki

Kitako kutwa sibaki, uzembenikaonesha,
Ulegevu hauliki, matumbo ukakutosha,
Ukata haukutoki, ukunguni ukibisha,
Yabidi nitarazaki, wanangu nikawalisha.

Kwa njaa hakukaliki, masumbuko yakaisha,
Ikwandamapo hilaki, uvivuwakebehisha,
Mwenyezi hakubariki, uvivukikadamisha,
Yabidi nitarazaki, wanangu nikawalisha.

La bidii nahakiki, hata liwe la kuchosha,
Hilo moja litabaki, mja akilidumisha,
Bidii hainitoki, kama najibidiisha,
Yabidi nitarazaki, wanangu nikawalisha.

Nitazipata miliki, sufufu zikanitosha,
Adui awe chuki, jasho langu kumtisha,
Niishi siabiki, nipendezwe na maisha,
Yabidi nitarazaki, wanangu nikawalisha.

Daima hawasumbuki, wanangu nikiwalisha,
Laana hainifiki, Mola anineemesha,
Milele niage dhiki, ukata kudidimisha,
Yabidi nitarazaki, wanangu nikawalisha.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!