Wimbo Wangu Narudia

Usichoke kusikia, mara nyingi kikwambia,
Sikereke itikia, wimbo wangu kikwimbia,
Sifoke kanirukia, vibovu kikuimbia,
Wimbo wangu narudia, nakuenzi malkia.

Hoja ziwe za kitoto, nikorome kama chura,
Ninganena shotoshoto, nitabasamu ja jura,
Zingatia wangu mwito, kakuone japo sura,
Wimbo wangu narudia, nakuenzi malkia.

Hiyo ngozi kahawia, tuseme tu chakuleti,
Na sauti lotulia, narudia sikuati,
Kila langu asikia, mikono mejizatiti,
Wimbo wangu narudia, nakuenzi malkia.

© Okelo w’Esonga
(Malenga Mtafunamiwa)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!