Siti Umenibeza

Nina mengi ya kutenda, yasiyokosa mkazo,
Si haba nimekulinda, kwa upeo wa uwezo,
Lakini unavyodinda, umeonesha mchezo,
Siti ninavyokupenda, malipo yako mawazo.

Usiku kucha nawaza, si haba hata mchana,
Kwa swifa umeniweza, la ziada ndilo sina,
Hatima umenikwaza, yasokomaa navuna,
Siti sasa wanibeza, umeona sijafana.

Kumbuka yaliyopita, tena nilivyokufaa,
Hujaona nimesita, kiwango utapumbaa,
Sasa umezua vita, ugomvi ukautwaa,
Siti sana nimetweta, tena siha kusinyaa.

Sijakosa lilo jema, kwa hilo kunipendea,
Siku hizo nilivuma, sana nikinyenyekea,
Hujawa na la huruma, jema ukanitendea,
Siti una la hujuma, kwa kasi linaenea.

Ulinipenda awali, sasa mengine wazua,
Huna sababu halali, fitina kuipakua,
Umeigeuza hali, ukawa wanitandua,
Siti huna la ukweli, kwa hilo tukatatua.

Chema hakijawa chema, kimeingia mchanga,
Imeshakuwa daima, mila yako ni kupinga,
Nilikwonesha hishima, ukalipa kunitenga,
Siti umenisukuma, kwa mengi unayolonga

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!