Nakula kwa macho

Ninapigiya kayamba, kwa sauti wastani,
Mwenzenu naimba imba, nikiwa huku pembeni,
Na leo sina kilemba, wala mambo hamsini,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.loo

Mwili wangu kama mamba, makunyanzi ya mwilini,
Kitambo siku za rumba, hungenitowa dansini,
Na hata kuruka Kamba, nilikuwa namba wani,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Nakumbuka huko Pemba, tulikaa baharini,
Hatungevaa mitumba, tuendapo harusini,
Tena hata kujipamba, tulishindana jamani,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Leo misuli mitumba, nguvu yake wastani,
Kutembea ninaimba, nayumba yumba njiani,
Uzee ushaa niramba, ushaningiya mwilini,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Wasichana wenye namba, niliwafurahisheni,
Kila siku kujibamba, nilipata afueni,
Niliwachezesha rumba, kuzeeka sikudhani,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Japo ninatamba tamba, si kama hapo zamani,
Hata kuicheza rumba, ni hapo kwangu chumbani,
Leo mavazi mitumba, mpya ninunue lini?,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Vijana mnao tamba, mlo na nguvu mwilini,
Muda wenu kujigamba, upo ni leo jamani,
Leo yenu ina bamba, kesho yenu ni usoni,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

Nahitimisha kurumba, “rangile” nina Amani,
Ninaitamani rumba, naangalia kwa mboni,
Roho safi kama pamba, mie sina walakini,
Leo nakula kwa macho, wenye nguvu sikieni.

© Joel Mburia

Maoni 4

Futa Jibu Futa Jibu

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!