Pesa zina Mwisho

Leo mwinyi utajike, bila kuwa na la shari,
Taji kubwa ujivike, uwanie umahiri,
Wataka ubainike, zijulikane habari,
Pesa zina mwisho wake, fukara huwa tajiri.

Machungu yafikirike, yawezekana yajiri,
Sikupashi uudhike, la ukweli utakiri,
Endapo yakafanyike, jua niliyabashiri,
Pesa zina mwisho wake, fukara huwa tajiri.

Langu dogo usitake, kunipenda ni hiari,
Hutaki ninufaike, wanelekeza kaburi,
Ni leo tu niinuke, ningali ninayo ari,
Pesa zina mwisho wake, fukara huwa tajiri.

U mwinyi usinicheke, huenda nikanawiri,
Nataka ieleweke, nisiweke liwe siri,
mkata hakosi lake, kama hanazo dinari,
Pesa zina mwisho wake, fukara huwa tajiri.

Iole kesho ifike, inafika isubiri,
Dunia ibadilike, ukose jema la heri,
Fukara wasiteseke, wabaki wakishamiri,
Pesa zina mwisho wake, fukara huwa tajiri.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!