Swifa Zako si Adimu

Naabtadi awamu, wasifu hadi pomoni,
Nakupenda madhulumu, subirazo maidani,
Staha waikadimu, nakshi yako tungoni,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Ushopoapo nudhumu, twajitenga faraghani,
Twakujuwa mahashumu, u mweledi wa amani,
Huna bee wala mimu, japo u mwinyi bongoni,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Huna zako darahimu, yamekukepa mapeni,
Umejaliwa ghanimu, ukabaki u laini,
Megubikwa ukarimu, taadhima huighani,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Umepambwa uharimu, kukomaa ukubwani,
Vema umestakimu, utepetevu hunani,
Muhali wakutuhumu, dhahiri wamebaini,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

Weledi wamezuumu, kukujua kwa undani,
Busara waifahamu, ustawi kutamani,
Imefifia dhulamu, hupenda kutamakani,
Swifa zako si adimu, kama kito cha thamani.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!