U Nami Sahibu

Huu wako wema, kwangu huwa ni hisani,
Napenda hekima, pakubwa huniauni,
Huna la hujuma, sana ninakuamini,
U nami sahibu, nami nitakuwa nawe.

Kamwe hunibezi, una mengi ya fadhili,
Mwenyewe siwezi, kufanikiwa muhali,
Umetenda kazi, vishindo umehimili,
U nami sahibu, nami nitakuwa nawe.

Kwangu ni furaha, kwa matendo yako mema,
Heri njema siha, itakufaa daima,
Kwako iwe raha, tuzo kwa yako heshima,
U nami sahibu, nami nitakuwa nawe.

Nimependa hali, kwa hiyo yako huruma,
Watu unajali, urafiki wako mwema,
Wasema ukweli, maneno yako yavuma,
U nami sahibu, nami nitakuwa nawe.

Nitakuwa nawe, kukushukuru kwa yako,
Katu siwi la kiwewe, imekwisha hamaniko,
Langu ulijuwe, nimependezwa na lako,
U nami sahibu, nami nitakuwa nawe.

Hongera mwandani, umenitunza vizuri,
Ukawa makini, kwa kunitakia heri,
Sasa nakwamini, mja asiye kiburi,
U nami sahibu, nami nitakuwa nawe.

© Kimani wa Mbogo 

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!