Huu ni Wangu Waadhi

Litendwalo ulitende, liwalo la maadili,
La kuudhi usipende, unalotenda ujali,
Lililo jema liunde, tena useme la kweli,
Huu ni wangu waadhi!

Uliwate la fitina, hisani ikupendeze,
Kisha koma kujiona, mara nyingi unyamaze,
Jiepushe la laana, wakuu wako watuze,
Huu ni wangu waadhi!

Tenda wema nenda zako, la kujisifu ukome,
Si la hoja tambuliko, mwenyewe ukajiseme,
Lilalo jema la kwako, kwa wengine ukavume,
Huu ni wangu waadhi!

Ya wakuu zingatia, si utakalo kutenda,
Tena muhimu tabia, jina jema kuliunda,
Yalo shwari kutimia, si lilo baya kuwinda,
Huu ni wangu waadhi!

Ni muhimu la heshima, kama ada ya maisha,
Kwa kutenda na kusema, taadhima inatosha,
Ukisema la hikima, yalo mema hukupisha,
Huu ni wangu waadhi!

Mfae ale mkata, uwezavyo kumwauni,
Si njiani kumpita, kwa mashaka maishani,
Mjali anayetweta, umpambe kwa hisani,
Huu ni wangu waadhi!

Usimbeze adui, hatakosa wake wema,
Huwa mwema ale mui, usimwoneshe hujuma,
Wako mwema humjui, atakufaa hatima,
Huu ni wangu waadhi!

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!