Jungu Imara

Kwa maji yenye kunywa, lihifadhi kwenye jungu,
Iituliza yetu vinywa, ya kumeza mate chungu,
Na maovu tulisinywa, kikemea kwa ukungu,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Jungu tulilopikia, chakula kikaivana,
Moto wetu kufukia, chakula kutokotana,
Na jifya kuijikia, jungu letu kulibana,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Jungu tuliloliumba, kwa miaka na mikaka,
Nakumbuka tukiimba, tumewacha utabaka,
Na migodi tukachimba, maji safi tulitaka,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Tuliamka asubuhi, siku hiyo mahabubu,
Kabla ya jua kuwahi, mabibi na hata babu,
Kwa makini walitusihi, kwenenda kitaratibu,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Maji yetu lichotea, na chakula kukitwaa,
Punde nyumbani rejea,aaaahhh kwenye kisiki lijikwaa,
Jungu vichwani regea, maji vichwani kupwaa!
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Lo! Jungu mebaki vigae, lisalia kugombana,
Kipi tena kitufae, kwa vigae lipigana,
Chozi letu litujae, kwa matusi likinzana,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Amani haipo tena, insi geuka wanyama,
Merejea ulitima, kujila nyama kwa nyama,
Mesahau na ujima, kuuana kwa unyama,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Maji yaliyo uzima, hayapo mekaukana,
Jifya liletalo sima, halipo mefukamana,
Kwenye sumu twasimama, na matumbo kuitana,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango.

Aaaaha!
Kwa mababu kutujia, suluhu lipatikana,
Tulibuni sufuria, chakula kutokotana,
Kuwapata mabaharia, kiu yetu kukatana,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Sufuria nayo ya chuma, ligawana nusu mkate,
Ikawa mwisho wa Juma, twameza sote kwa mate,
Tusahau ilo hujuma, kwa umoja tupakate,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Mwisho wangu ni himizo, ngao yako ndio chuma,
Ngao yenye uwezo, kura yako kuichuma,
Na kuondoa vikwazo, michafuko na dhuluma,
Iweje jungu imara, kupasuka kwenye mlango?

Malenga mlengajitu
Mutambo M Brian
University of Eldoret

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!