Majisifu Hayafai

Lako huwa ni kusema, tena wingi wa madai,
Sijaona lako jema, sifa zako hazifai,
Unawania kuvuma, kwako sifa hazijai,
Huna mbele huna nyuma, majisifu hayafai.

Heri uombe Latifu, kukwongeza maarifa,
Hunalo la ubunifu, kukupandisha wadhifa,
Usiseme ni hafifu, hino yangu taarifa,
Una haki kujisifu, japo hutoshi la swifa.

Kwa hizo hufaidiki, vyovyote hazikutoshi,
Lako litakuwa dhiki, faraja haikupishi,
Kwa sifa hufahamiki, isipokuwa ubishi,
Sifa haziwi riziki, ni kazi bure bilashi.

Kila mwendo ni hatua, hukuzaliwa mwalimu,
Kwa sasa utatambua, pasipo kutulaumu,
Si haba umeyazua, mambo mengi yasodumu,
Usijisifu kujua, kwa mambo usofahamu.

Tenda hili tenda lile, wengine kukuswifia,
Uyasubiri yajile, kukujalia Jalia,
Utakapo sifa tele, lazima ukawania,
Sifa haziwi mishale, wengine kuwadungia.

Lielewe kugundua, huenda likakufaa,
Muhimu kulitambua, sahibu ukanyamaa,
Dhahiri utalijua, la muhimu kukujaa,
Huko kujifaragua, hakuna la manufaa.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!