Moraa

Mapenzi yamenikwida, siwezi nikapumua,
Nampenda huyu dada, jina aitwa Moraa,
Kumpenda ni kaida, kwa mia asilimia.

Kwa mia asilimia, nampa yake heshima,
Sitaki aje jutia, na moyo kumsimama,
Moyoni mempokea, dhambi uongo kusema.

Dhambi uongo kusema, hakika ninampenda,
Kisura mwenye heshima, simchezi ja kandanda,
Ukweli wangu nasema, toka moyo mempenda.

Toka moyo mempenda, kwa mwengine sitamani,
Siku mingi mempenda, namuenzi maishani
Sitaki nije uponda, moyo wake asilani.

Moyo wake asilani, ja yai meudekeza
Yai lipo mkononi, leo siendi kucheza,
Amani ipo moyoni, kama halitateleza.

©Justine Bin Orenge

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!