Fumbo ni Kufumbua

Fumbo si kulumba, fumba kutambua,
Fumbo si kuamba, fumbo kuchambua,
Fumbo si kufumba, fumbo kufumbua.

Fumbo si kusita, fumbo ni hatua,
Fumbo si kuota, fumbo kugutua,
Fumbo si matata, fumbo kutatua.

Fumbo si kutaja, fumbo ni kujua,
Fumbo si daraja, fumbo mwanga jua,
Fumbo si kiroja, fumbo ni rajua.

Fumbo si kusema, fumbo kuamua,
Fumbo si kuvuma, fumbo sisimua,
Fumbo si kukwama, fumbo kung’amua.

Fumbo si kutunga, fumbo kugangua,
Fumbo si kupanga, fumbo kutungua,
Fumbo si kuwinga, fumbo kuzingua.

Fumbo si kufoka, fumbo kupakua,
Fumbo si kutaka, fumbo kupekua,
Fumbo si kuwika, fumbo kunyakua.

Fumbo si kushinda, fumbo kutandua,
Fumbo si kudinda, fumbo kugundua,
Fumbo si kuwinda, fumbo kupindua.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!