Kidege changu Milie

Nasema yalo moyoni, nimezama mapenzini,
Metamalaki moyoni, unatawala mawazoni,
Usiku upo ndotoni, mchana u mawazoni,
Kidege changu Milie, ninakupenda kwa dhati.

Siku baada ya siku, nakuwazia kipenzi,
Hata kulala usiku, nakufikiri mpenzi,
Leo kesho kila siku, talitunza letu penzi,
Kidege changu Milie, ninakupenda kwa dhati.

Moyoni sina wahaka, kindumbwendumbwe meshinda,
Siniekee mipaka, nakuomba wangu kinda,
Yapendeza kukumbuka, moyoni navyo kupenda,
Kidege changu Milie, ninakupenda kwa dhati.

Milie u avidadi, nakupa mia fi’ mia,
Sura yako maridadi, mbioni inanitia,
Kukupenda sina budi, mtimani mekutia,
Kidege changu Milie, ninakupenda kwa dhati.

Roho yangu taabani, kisura changu Milie
Nakuenzi asilani, siniache niduwae
Mekuhifadhi moyoni, nakudekeza ja yae
Kidege changu Milie, ninakupenda kwa dhati

© Justine Bin Orenge

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!