Nitazoea

Moyoni nimeumia, kupenda nisipopendwa,
Moyo unanikimbia, sikudhani nitatendwa,
Kweli nilimwaminia, sikujua sikupendwa
Sawa nimeshaumia, lakini nitazoea.

Niliambia dunia, kumpata ni bahati,
Kote nilitangazia, nimpendavyo kwa dhati,
Huo muda ningejua, ngesoma hata gazeti
Sawa nimeshaumia, lakini nitazoea.

Maishani melilia, mapenzi yasokuwepo,
Mbali nayatupilia, machoni ‘jifanye popo,
Mbili nitafikiria, mtimani nipendapo,
Sawa nimeshaumia, lakini nitazoea.

Hili limeshatokea, kung’atuka sina budi,
Moyoni navumilia, maumivu niyazidi,
Mazuri nitamwombea, asipate wa komedi,
Sawa nimeshaumia, lakini nitazoea.

© Justine Bin Orenge

Maoni 3

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!