Tazama… 

Tazama umeshaudhi, ukawa kwangu hufani,
Tazama nakukabidhi, ushauri wa mwandani,
Tazama wangu waadhi, uelewe kwa makini.

Tazama ulivyotenda, mengi ya Kushangaza,
Tazama unakoenda, mashaka yakuongoza,
Tazama unavyoranda, kikakuandama kiza.

Tazama huna mazuri, yakuandame swahibu,
Tazama huna la siri, ulifite ja dhahabu,
Tazama hizo athari, zimekuletea tabu.

Tazama huzingatii, wambiwalo hulitendi,
Tazama huniambii, unambie hunipendi,
Tazama hunitakii, mema yalete ushindi.

Tazama unavyolumba, lisemwalo hubaini,
Tazama unavyoamba, lako ni la walakini,
Tazama wanavyofumba, wakiwa nawe wazoni.

Tazama huna huruma, utendavyo siamini,
Tazama mengi yamekwama, kwa huo wako uhuni,
Tazama sasa tazama, swahibu huna hunani.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!