Mapenzi Kizunguzungu

Nilimpenda malaika, na kumpa yangu yote,
Kila pembe nikawika, kumvisha hata pete,
Na huzuni ikifika, tulilia sisi sote,
Mapenzi kizunguzungu,inapasa tahadhari.

Tulikesha siku kucha,na kuzama kwa mahaba,
Penzi letu likachacha, kanibusu mara saba,
Nilihofu kumuacha, heri nife kwa niaba,
Mapenzi kizunguzungu,inapasa tahadhari.

Kila kitu tulifanya, tukanena tuloweza,
Nami nikamkanya, sidhubutu kuniliza,
Hapana lilotusinya, lipendana kumaliza,
Mapenzi kizunguzungu, inapasa tahadhari.

Myaka kenda myaka rudi, tulizidi letu penzi,
Tukasema tuna budi, ndoa yetu kuienzi,
Niliona ni kusudi, Mola kunipa mwenzi,
Mapenzi kizunguzungu, inapasa tahaehari.

Naogopa na kusema, penzi letu kulemaa,
Malaika kunitema, kaniwacha meduwaa,
Kuwa hanitaki tena, nilibaki mezubaa,
Mapenzi kizunguzungu, inapasa tahadhari.

Niliona ni mateso, kimwana kunipa teke,
Nikalala bila leso, kuukosa ‘bavu wake,
Mwendo wa kimasomaso, nayo pia haiba yake,
Mapenzi kizunguzungu, inapasa tahadhari.

Nimefika kwa tamati, naweleza nyi vijana,
Mapenzi kweli bahati, huweza kukosekana,
Labda kwenye mauti, sio tu kugombana,
Mapenzi kizunguzungu, inapasa tahadhari.

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!