Kaka na Dada

KAKA:
Dada leo umenuna, hata sasa hujakula,
Ni kipi kinakukuna, wakati wanza kulila,
Shida ni kupashaanaa, hasaa iwe ya hila,
Sasa pasua mbarika, ni tayari kusikiza.

DADA:
Kaka wacha chokozi,fyatoa hilo domo lako,
Wajifanya uu mwokozi, kwa hicho  kisemi chako,
Mimi kamwemwe sio bozi, kutaka usaidizi kwako,
Usilolijua jamani, halihusu ndewe sikio.

KAKA:
Mbona watoa makali, shida ni kuelewana,
Hata na yangu kauli, imekuwa kubishana,
Na mambo kuwa kikuli, ila ya kutangamana,
Dada umedhoofu, ila wazidi nificha.

DADA:
Kweli ni makuu, ya kujitia kitanzi,
Niweke wapi nafuu,katika wako ulinzi,
Ni yule bwana mkuu, niliyeozwa maajuzi,
Megeuka gumegume, kunisamba na mateke.

KAKA:
Sasa nimepata mwanga,mumeo mekufukuza,
‘nimulika ja kitanga,ndoani hukutimiza,
Bwanayo kitangatanga, kumuenzi hukuweza,
Mke na mme hakika,ni kupendana kiundani.

DADA:
Wacha ‘yo matusi, nilikuwoni mwanzoni,
Nimeshikwa na virusi, ila wewe hauoni,
Mimba hino ibilisi, menifanya wacha shule,
Nimebaki nikilia, kwa sababu sina nia.

KAKA:
Dada kweli nisamehe, najutia nilokuenda,
Tulikuwa kina yakhe, kukuoza tukupenda,
Heri twende kwa mashehe, tutubu miaka kenda,
Mkuki ni kwa nguruwe,kwa binadamu mchungu.

DADA:
Usemayo ni ya kweli, kusamehe nimewahi,
Nataka kwenda skuli, waalimu niwasabahi,
Niwe ni mwenye akili, fanya mambo kisahihi,
Niwe ni mwenye akili, fanya mambo kisahihi,
Kuzaa mwana si kazi, kazi kubwa ni malezi.

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!