Nyuki Joka Watuliza

Swali hili naliweka, kila mtu tafakari,
Mzigo huu kuzuka, mimi bado nafikiri,
Nyuki hawa wamefika, wana silaha hodari,
Ni nani ananimaliza, kati ya nyuki na joka?

Nimevamiwa shambani, nao nyuki wakatili,
Nakimbilia pembeni, kuepuka na makali,
Mwenzenu nimo mashakani, kunyakuliwa hata mali,
Ni nani ananimaliza, kati ya nyuki na joka?

Nyuki  wamo mzingani, masikini nateseka,
Nafikiri la nyumbani, usiku ukinifika,
Wazo langu akilini, kuwafurusha haraka,
Ni nani ananimaliza, kati ya nyuki na joka?

Japo nyuki wanatisha, watuletea asali,
Nitawafukuza kisha, nifurahie asali,
Moto wangu nauwasha, kuwamaliza katili,
Ni nani ananimaliza, kati ya nyuki na joka?

Umevamiwa mzinga, pindi nyuki kutoweka,
Nalo joka la upanga, asalini kujitwika,
Jiwe langu kulilenga, kwa ukali linawika,
Ni nani ananimaliza, kati ya nyuki na joka?

Uhuru wangu sioni, hali yangu kawaida,
Joka hili ni mhuni, lanitia kwenye shida,
Lanifuata na mwituni, nililishe kila muda,
Ni nani ananimaliza, kati ya nyuki na joka?

Akili imenikwama, mwenzenu nasononeka,
Lini joka litahama, mi niwache kuteseka,
Japo mambo ni mrama, majoka yafurahika,
Ni nani ananimaliza, kati ya nyuki na joka?

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!