Hana Soni

Nimo sasa safarini,kuelekea shuleni,
Begi langu mgongoni,najituliza garini,
Mkanda uu kiunoni, metulia nii kitini,
Mwizi huyu soni hana,kanipora mara tena

Abiria wamejaa, wengi wao manambaa,
Gari hili mechakaa,lafanana ja makaa,
Watu hawa ni kichaa,meniwacha kuduwaa,
Mwizi huyu soni hana,kanipora mara tena.

Kondakta anikabili, sijalipa na nauli,
Nimeshikwa na kikuli,nimepoteza nauli,
Amejawa na makali,mtu huyu baradhuli
Mwizi huyu soni hana,kanipora mara tena.

Basi nashushwa ndiani, mwenzenu sina sinani,
Begi langu silioni,menyakuliwa na nyani,
Ninetiwa matesoni,mwendo maili ‘shirini,
Mwizi huyu soni hana, kanipora mara tena.

Shuleni nimechelewa, walimu kutoelewa,
Na mwizi kusingiziwa,wamedhani nimelewa,
Karo yangu kutolipwa,mizigo nimelemewa,
Mwizi huyu soni hana,kanipora mara tena.

Mlo wezi nawaonya,mmekuwa mkisinya,
Hata muwe kina nyanya,mnoiba hata nyanya,
Hivi sasa nawakanya, kuwaudhi wanakenya,
Mwizi huyu soni hana,kanipora mara tena.

Nimefika kwa tamati, meishiwa na wakati,
Mwizi akiiba shati,hasiti kuiba suti,
Akiiba nayo koti, mshitaki kwenye korti,
Mwizi huyu soni, hana kanipora mara tena.

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!