Nasamehe Sisahau

Litujia kwa usiku, nilikuwa nimelala,
Jumapili hiyo siku, nakumbuka kwa mandhila,
Sisemi mie ja kasuku, kilio changu ni cha hila
Nasamehe we jambazi, sitokusahau aushi.

Ilikuwa saa tano, mkabisha mlangoni ,
Linena kwa minong’ono, bastola mgongoni,
Mlikuwa watu tano, kuitisha milioni,
Nasamehe jambazi we, sitokusahau aushi.

Baba kawa wa kwanza, kwa kudai hela hana
Lil’pua risasi kwanza, kusikika jiji pana,
Mama kapiga ukwenza, baba kweli hakupona,
Nasamehe jambazi we, sitokusahau aushi.

Ilikuwa ni majonzi, baba kufa nikiona,
Katamani kujitanzi, mezirai kando nina,
Kageuka kuwa simanzi, furaha lodhaniana
Nasamehe jambazi we, sitokusahau aushi.

Japo kuwa nasamehe, sitasahau kabisa,
Hata niwe kamwe shehe, msimamo sitotikisa,
Tanakili na tarehe, ’likuwa tarehe tisa,
Nasamehe jambazi we, sitokusahau aushi.

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!