Si Chokoraa ni Mtu

Mja huyu mwenzetu, mbona tunamudhulumu.
Jama Tunakosa utu, hilo nanyi lifahamu.
Piya na yeye ni mtu, tumutolee ugumu.
Si chokoraa ni mtu, ana akili timamu.

Japo huwa anaranda, msimwone ni jeuri.
Kuchokora hakupenda, na haoni ufahari.
Wazaziwe walipenda, wakamtenga kisiri.
Si chokoraa ni mtu, ana akili timamu.

Ni vipi atafaidi, mkimtusi jamani.
Kumwita yeye gaidi, anapopita ndiani.
Kumwona kama hasidi, ‘kiomba barabarani.
Si chokoraa ni mtu, ana akili timamu.

Matambara Huyavaa, senti akiombaomba.
Nanyi mboko mnatwaa, mgongoni kumwamba.
Huchepuka akilia, kwa uchungu ulomkumba.
Si chokoraa ni mtu, ana akili timamu.

Mwajifanya mna utu, kumbe nyinyi hayawani.
Mnawaona viatu, kuwacheka hadharani.
Ati wao sio watu, wanachokora pipani.
Si chokoraa ni mtu, ana akili timamu.

Kakomeni kuwasuta, wasalie masikini.
Kila unapowapita, matonge kwao rusheni.
Furaha kwao kinata, mtaenda mbali jamani.
Si chokoraa ni mtu, ana akili timamu.

Nikizidi kuandika,nahuzunika rohoni.
Kwa wingi nitalizika,machozi tele usoni.
Tamati hapa mefika,kalamu naweka chini.
Si chokoraa ni mtu,ana akili timamu.

© Mstahiki Zack

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!