Mwanadamu tenda Mema

Salamu zangu mwanzoni, kalamu ninaishika.
Wakenya niwajuzeni, uchungu ulonifika.
Nchi yetu ya zamani, mabaya yameifika.
Mwanadamu tenda mema, ukaepuke kiyama.

Wanadamu mumezidi, mumekuwa hayawani.
Machafu munayanadi, kotekote hadharani.
Mwafanya mso faidi, hamna tena hisani.
Mwanadamu tenda mema, ukaepuke kiyama.

Utuwapo spitali, ‘chai’ kwanza katoeni.
Kukutibu hawajali, bila kutoa mapeni.
Iwatishe yako hali, ndipo ulazwe wodini.
Mwanadamu tenda mema, ukaepuke kiyama.

Kifungua yako kazi, tajirike kibahati.
Watazua ya upuzi, uitwe ‘illuminati’.
Hata uwe na ujuzi, tajipotezea wakati.
Mwanadamu tenda mema,ukaepuke kiyama.

Polisi barabarani, hongo wanaitakeni.
Wanazua wao zani, manamba wapo tabuni.
Madereva watoeni, au jela wende ndani.
Binadamu tenda mema, ukaepuke kiyama.

Mabinti munawabaka, mwawakosea heshima.
Aibu munawavika, kwa zenyu nyingi dhuluma.
Kimaliza mwawacheka, kuwadharau daima.
Mwanadamu tenda mema, ukaepuke kiyama.

Tajikuta matatani, kifika kiyamani.
Utajutiya jamani, takuhukumu manani.
Takosa kwenda peponi, uishiliye motoni.
Binadamu tenda mema,ukaepuke kiyama.

Namba nane naishia, nahofia gazetini.
Ningetunga beti mia, wenzangu ningewahini.
Hili pia nahofia, litachakaa kapuni.
Mwanadamu tenda mema, ukaepuke kiyama.

© Mstahiki Zack 

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!