Mali

Ukiwa nayo tumia, lakini sio kufuja,
Usiishi kwa udhia, mali yako tayafuja,
Kosa hivi utalia, na taabu zitakuja,
Mali ni kitu kizuri, kibaya kinapofujwa.

Mitego i mingi sana, ya kuyafuja maliyo,
Anasa ziko kazana, zizije bananga moyo,
Changudoa wengi sana, walenga yako yaliyo,
Mali ni kitu kizuri, kibaya kinapofujwa.

Wasiojiweza wape, kamwe usiwe mchoyo,
Usijewaita kupe, kawavunja zao nyoyo,
Kitachowafaa wape, shukurani zi kwa moyo,
Mali ni kitu kizuri, kibaya kinapofujwa.

Magari ya kifahari, majumba tayanunua,
Tayaonea fahari,  hayataki mchupia,
Litakuhiliki gari, jamii yako talia,
Mali ni kitu kizuri kibaya, kinapofujwa.

Usipoepuka raha, mali tayafuja yote,
Upate mwisho karaha, ‘lilotaraji sipate,
Takosa nayo furaha, maradhi nayo upate,
Mali ni kitu kizuri, kibaya kinapofujwa.

Maradhi yatakusonga, utatike kitandani,
Kamwe tena hutaringa, utakuwa taabani,
Mauti yatakutinga, uozee kaburini,
Mali ni kitu kizuri,kibaya kinapofujwa.

© Samuel Nguru Mwangi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!