Maisha Shuleni

Maisha raha shuleni, lakini mchache muda,
Usidhani sebuleni, utumie vyema muda,
Sipotokee shuleni, utauharibu muda,
Maisha shuleni mema, lakini muda mchache.

Watii walimu wako, mitihani utapita,
Heshimu wazazi wako, kisha vyema utapita,
Potosha tabia zako, mtihani hutapita,
Maisha shuleni mema, lakini muda mchache.

Simsahau Muumba, unapoifanya kazi,
Masomo kama nyumba, hayajengwi kwa ubozi,
Msingi mwema wa nyumba, haujengwi kwa upuzi,
Maisha shuleni mema, lakini muda mchache.

Utakapokwisha muda, utaelekea wapi?
Ukiupoteza muda, utaelekea wapi?
Utakosa nayo ada, mwisho uyale makapi,
Maisha shuleni mema, lakini muda mchache.

© Samuel Nguru Mwangi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!